Tuesday, January 22, 2013

JENGO LAANGUKIA MAGARI 23 DAR

Jengo linalotumika kwa ajili ya maegesho ya magari ya watu binafsi katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani Ubungo (UBT)  jijini Dar es Salaam, limeporomoka na kuangukia magari zadi ya 23 na bajaji tatu na kuharibika vibaya na kujeruhi watu wawili.

Kutokana na ajali hiyo, ambayo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ametembelea eneo la tukio na kutoa tamko la kutaka waliohusika na uzembe huo wachukuliwe hatua za kisheria.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda ya Dar es Salaam, Amir Ponja, akizungumza na waandishi wa habari kituo hapo alisema tukio hilo lilitokea majira ya jana saa 11:30 alfajiri.

Alisema watu waliojeruhiwa majina yao hayajafahamika na kwamba walikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu.

Meneja wa kituo hicho, Juma Iddi, alisema kuwa zoezi la ubomoaji wa majengo katika kituo hicho linaendelea kwa ajili ya kupisha mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (Dart).

Hata hivyo, Iddi alisema kuwa mhandisi aliyepewa kazi hiyo hakueleza kama kuendelea kuegesha magari eneo hilo kunaweza kuleta madhara kama yaliyotokea.

Watu walioshudia tukio hilo waliulaumu uongozi wa kituo hicho kwa kuwalazimisha watu kuegesha magari yao kwenye eneo ambalo ubomoaji ulikuwa ukiendelea.

“Nilipoingia na gari langu kwenye lango kuu, nilielekezwa kuegesha gari kwenye eneo hilo la ajali na wakati najiandaa kuzima gari, ghafla nikaona nguzo na kuta zinaanguka, nikachomoka kwenye gari na kukimbia,” alisema Peter Gamba.

Gamba ambaye ni mmiliki wa gari namba BYY 362 aina ya IST alisema kuwa hakupata majeraha makubwa ila alichubuka kwenye mkono wake wa kushoto.

Mnyika alipotembelea eneo la tukio, alisema kuwa serikali inapaswa kuingilia kati kuepusha maafa zaidi kutokea katika kituo hicho kutokana na utaratibu unaotumika wa kuvunja majengo huku kikiendelea kutumika.

Alisema kuwa ajali hiyo aliyoiita ya kizembe ni matokeo ya udhaifu wa serikali kutochukua hatua kwa wakati.
Alisema kuwa serikali  inatumia utaratibu mbovu kukihamisha kituo hicho kwenda Mbezi Luis huku  kikiendelea kutumika.

Alisema kuwa, tangu mwaka 2011 aliishauri serikali pamoja na kupeleka hoja binafsi kwenye Baraza la Jiji, aliitaka serikali kufanya maamuzi ya haraka kuainisha mapema maeneo ya kituo hicho yatatumiwa na Dart.


 

No comments: