Mbunge wa Ziwani, kisiwani Pemba, Ahmed Juma Ngwali (CUF), amefunguliwa jalada katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam, akituhumiwa kuvunja ndoa ya mfanyabiashara wa mjini Unguja na kutorosha watoto wawili nchini kwenda Canada, kinyume cha sheria.
Ngwali anatuhumiwa na mfanyabiashara huyo, Khalfan Said Chondoma,
mkazi wa Saateni, kisiwani Unguja, kuingilia ndoa yake na kusababisha
kuvunjika na hivyo kupata mwanya wa ‘kumpora’ mkewe.
Pia anatuhumiwa kutorosha watoto wa mfanyabiashara huyo msichana
(8) na mvulana (9) na kuwapeleka Canada baada ya kuwabadili ubini halali
wa baba yao mzazi na kuwapachika ubini wa mbunge huyo.
Khalfan aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuwa
aliripoti suala hilo katika kituo cha polisi Oysterbay na kufungua
jalada namba OB/RB/21545/2012.
Khalfan (31), analalamikia kutoroshwa kwa watoto wake chini ya
himaya ya wazazi na kuwa kabla ya matukio hayo, Ngwali alikuwa rafiki
yake aliyekuwa akimtembelea nyumbani, lakini hakujua kuwa alikuwa ana
lake moyoni dhidi ya mkewe.
Alidai kuwa alikuja kubaini hilo baada ya kuanza kuona uhusiano mzuri uliokuwa kati yake na mkewe awali ukibadilika ghafla.
Khalfan alidai uhusiano kati yake na mkewe uliendelea kuwa mbaya hadi ulipotokea mtafaruku mkubwa kati yao.
Alidai kufuatia mtafaruku huo, mkewe aliondoka nyumbani bila kupewa talaka na kwenda nyumbani kwa wazazi wake mkoani Tanga.
Khalfan alidai wazazi wake waliingilia kati mgogoro huo, lakini
yeye akashikilia msimamo wake kwamba, ili ampokee na kuendelea kuishi
naye sharti akubali kutofanya kazi kwa kuwa hana uwezo huo kutokana na
elimu yake kuwa ya darasa la tano.
Alidai mkewe aliendelea kupinga sharti hilo na hivyo kukataa kurejea kwake.
Kwa mujibu wa Khalfan, wiki chache baadaye alisikia kuwa mkewe ameolewa na mbunge huyo bila kumpa talaka.
Alidai kuwa watoto wake walitoroshwa kwenda Canada, Oktoba 30, mwaka jana, baada ya mbunge huyo kuwapachika ubini wake.
“Aliwabadilisha ubini wao halali na kuwaita (anataja majina yao),”
alidai Khalfan. Alidai hadi sasa watoto wake bado wanaishi Canada,
ambako wao na mama yao wamejitambulisha kama wakimbizi. “Sijui
wamejilipua kama wakimbizi wa nchi gani, maana Tanzania hatuna
wakimbizi,” alidai Khalfan.
Hata hivyo, alidai kuwa taarifa alizonazo ni kuwa watoto wake
walitakiwa kurudi nchini Novemba 7, mwaka jana, lakini haijulikani
kwanini hadi sasa hawajarudi.
Alidai kufuatia kitendo hicho, aliwasiliana na Mtandao wa Polisi wa
Kimataifa (Interpol) nchini, ambao aliwakabidhi vielelezo vyote
vinavyohusiana na shauri hilo. Khalfan alidai Interpol walikwenda
Zanzibar, pamoja na mambo mengine, walichukua vivuli vya pasi za
kusafiria zilizoandikwa ubini bandia wa watoto hao.
Alidai baada ya kuchukua vielelezo hivyo, Interpol walimhakikishia kuwa wanaendelea kufuatilia suala hilo.
Khalfan alidai anachokitaka ni kujua Ngwali ana haki gani kisheria
kukaa na watoto wake, pia serikali ifahamu kile alichokiita “udhalimu”
aliodai kufanywa na mbunge huyo na vilevile anataka apewe watoto wake.
Khalfan alionyesha vielelezo mbalimbali, kikiwamo cheti cha ndoa
kuthibitisha kuwa alifunga ndoa na Aisha Machi 11, 2004; pia vyeti vya
watoto hao vya kuzaliwa kuthibitisha kuwa ni watoto aliowazaa na
mwanamke huyo.
KAULI YA MBUNGE NGWALI
NIPASHE jana iliwasiliana na Ngwali kwa njia ya simu, ambaye
alithibitisha watoto hao pamoja na mama yao mzazi, Aisha kuwapo Canada.
Ngwali alisema Aisha ni mkewe halali wa ndoa, lakini watoto hao ni wa Khalfan.
Alidai hakumbuki tarehe na mwezi aliofunga ndoa na Aisha, lakini
anachokumbuka ndoa yao ilifungwa miaka miwili iliyopita baada ya
mwanamke huyo kumkataa Khalfan kutokana na kumzuia kufanya kazi ya duka.
Ngwali alidai ndoa kati yake na Aisha ilifungwa wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, kwa idhini ya wazazi wa mwanamke huyo.
Ngwali alidai cheti cha ndoa kinachothibitisha kuwa alifunga ndoa
na Aisha kipo, lakini kwa kuwa yeye husafiri mara kwa mara, hawezi
kutembea nacho mkononi.
Alidai hakuwahi kuishi na watoto hao, bali walikuwa wakiishi na bibi yao mzaa mama Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.
Hata hivyo, alidai kuwa hakuishi muda mrefu na Aisha, kwani mwaka
jana mwanamke huyo alifanya hadaa na kuondoka kwenye himaya yake na
kwenda kuishi na watoto hao Canada, kinyume cha taratibu.
Alidai kuwa kufuatia kitendo hicho, aliuandikia barua Ubalozi wa
Canada, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Jeshi la
Polisi kuwaelezea kilichotokea kuhusiana na mwanamke huyo.
“Nilimwamini kama mke wangu, lakini akafanya kinyume,” alidai Ngwali.
Alidai awali, walipanga na Aisha kwenda Canada, akampa jukumu la
kutafuta viza, lakini akiwa bungeni, mwanamke huyo aliamua kuondoka
kinyemela kwenda nchini humo.
Ngwali alisema anamshangaa Khalfan kumsikia akimtuhumu kutorosha
watoto wake na kudai yeye hana shida ya watoto wa mtu mwingine, kwani
tayari anao watoto wanne aliozaa na mkewe wa kwanza.
“Huyu bwana anacholilia ni wivu tu wa mapenzi. Haya mambo
ukiyasikia ni ya ajabu. Kwani aliwahi kunitaka nimfidie. Hao watoto siyo
wangu, vipi unilalamikie mimi?” alihoji na kuongeza: “Anataka
kunichafulia jina.”
Alimshauri Khalfan kwenda mahakamani, akidai huko ndiko haki
inakotolewa badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari ili
kumchafulia jina, kwani kwa kufanya hivyo hakuna faida yoyote anayoweza
kuipata. Alidai pia anamshangaa Khalfan kumtuhumu kwamba, amebadili
majina ya watoto wake bila kuthibitisha tuhuma hizo.
Ngwali alidai kwamba ni jambo lisilowezekana kubadili majina ya watoto kwani ilitakiwa aende kufanya hivyo mahakamani.
Pia alidai tangu azaliwe hajawahi kwenda mkoani Tanga na watoto hao hawamo kwenye pasi yake ya kusafiria.
“Mimi hawa watoto siyo wangu. Ninao wangu wa halali. Kama kuna mtu
kabadilisha majina yao, mimi sijui. Na atoke mtu yoyote duniani
athibitishe hilo, nitawajibika,” alidai Ngwali na kuendelea:
“Yule mwanamke ana asili ya Kiarabu na Khalfan ana asili ya
Kiarabu. Mimi ni Mswahili. Hiyo ndiyo asili ya chuki na huyu bwana.
Kwamba, kwanini Mswahili aoe Mwarabu? Sasa tatizo hapa siyo watoto, bali
tumkomoe.”
Ngwali alidai kama ni uchungu, basi yeye ndiye anayeumia zaidi
kwani alikuwa akiwalipia watoto hao ada ya shule Shilingi milioni tatu
kwa mwaka.
“Hivyo, yote anayosema ni uwongo. Anataka aonewe huruma. Ni wivu tu
wa mapenzi ndiyo unaomsumbua. Kwa hiyo, hiyo story (habari). Ni watu
wanaogombea mwanamke na sote tumemkosa.”
Ngwali alidai sehemu kubwa ya maelezo hayo aliyatoa alipohojiwa na vyombo vya dola, ikiwamo interpol.
KAULI YA POLISI
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kinondoni, John Mtalimbo, alisema
taarifa za Khalfan kufungua jalada hilo katika kituo hicho alizisikia
jana, hivyo alimtaka mwananchi huyo kwenda ofisini kwake leo asubuhi ili
kujua suala lake lilipofikia.
Hata hivyo, alisema kwa jinsi lilivyo, suala hilo ni kubwa, ambalo
hata kama jalada lake lilifunguliwa katika kituo hicho, bado linahusiana
na Interpol. Pia NIPASHE ilijaribu kuwasiliana na Msemaji wa Jeshi la
Polisi nchini, Advera Senso, kueleza sababu za shauri hilo kuchukua muda
mrefu, lakini hakupatikana.
Alipopigiwa simu yake ya mkononi ilipokelewa na mtu
aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wake, ambaye alisema angemfikishia
bosi wake ujumbe wa kutafutwa na mwandishi.
No comments:
Post a Comment