Vitendo vya wizi katika Bandari ya Dar es Salaam vimeendelea kushika kasi na kuisababishia serikali kukosa mapato yake baada ya vigogo katika bandari hiyo kudaiwa kuiba kontena lenye madini aina ya Tantalite yenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 10.
Madini hayo yanapatikana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Rwanda na Burudi pekee na yamekuwa yakisafirishwa kutoka katika nchi
hizo kupeleka nje kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Kutokana na wizi huo ambao Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wameandika katika nyaraka zao kuwa una thamani ya Dola za kimarekani
22,000, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameagiza maofisa
waliohusika wakamatwe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kwa miezi minne
serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka serikali ya Rwanda kuhusu
kuwapo kwa mtando wa wezi wa madini hayo katika Bandari ya Dar es
Salaam.
Dk. Mwakyembe alisema kutokana na vitendo hivyo, juzi Balozi wa
Rwanda nchini alimpigia simu kumweleza kuwapo kwa tatizo hilo ambalo
limekuwa likilalamikiwa na kampuni na wafanyabiashara wanaosafirisha
madini hayo kupitia bandari ya Dar es Salaam.
“Balozi wa Rwanda aliponipigia simu kunieleza kuwa mawaziri wawili
kutoka Rwanda ambao ni Waziri wa Uchukuzi na Waziri wa Biashara watakuja
hapa nchini kujadili suala hili ambalo tayari makampuni makubwa
yameacha kupitisha madini hayo katika bandari ya Dar es Salaam,”
alisema.
Alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema, alifanya
ziara katika bandari hiyo akiwa na askari polisi na kukuta hujuma kubwa
zimefanywa na maofisa wa taasisi za serikali.
Alisema madini hayo ambayo thamani yake ni zaidi ya Dola za
Kimarekani milioni 10, lakini maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA)
wameandika katika nyaraka kuwa yana thamani ya dola 22,000.
No comments:
Post a Comment