Saturday, April 20, 2013

MAUAJI DAR, "MTU MMOJA AUAWA KIKATILI"


 kamanda wa polisi,mkoa wa kipolisi temeke engelbert kiondo

Mtu mmoja jijini Dar es Salaam ameuawa kinyama kwa kupigwa, kisha mwili wake kuingizwa ndani kiroba na kutupwa ndani ya mtaro wa maji. Mwili wa mtu huyo umeokotwa jana majira ya saa 2:00 asubuhi eneo la Nyamachoma Yombo Buza baada ya wakazi wa eneo hilo kusikia harufu kali kutoka kwenye mtaro wa maji machafu pembeni ya barabara ya Yombo.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo, walisema mwili huo wa mtu mwanaume ulikutwa ukiwa umewekwa ndani ya viroba viwili, kisha kutupwa kwenye mtaro kama takataka na watu wasiojulikana. Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina mama Hassani, alisema chanzo cha kugundulika ni harufu kali iliyokuwa ikitoka kwenye mfuko huo na kusambaa eneo lote. "Baada ya kusikia harufu, tulianza kusaka inatokea wapi, ndipo tulipogundua inatoka kwenye mzigo wa kiroba uliokuwa ndani ya mtaro wa maji," alisema mwanamke huyo.

 Alisema, kutokana na hali ya mzigo huo, walijua ndani yake kuna takataka, lakini walipoondoa kiroba hicho walikuta miguu ya mtu. Hata hivyo, walishindwa kuendelea kuondoa kiroba kingine na kuamua kuwaita polisi ili kwenda kuuchukua mwili huo. "Inaelekea mtu yule aliuawa siku tatu zilizopita nyakati za usiku, kwa sababu ndani ya kiroba alikuwa katika hali ya kuchuchumaa na mikono yake imefungwa kamba kwa nyuma," alisema mkazi mwingine Abubakar Saidi. Mashuhuda hao walisema askari polisi walifika eneo la tukio majira ya saa 4:30 asubuhi na kuuchukua mwili huo na kuupeleka kituo cha polisi Chang'ombe. Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema bado hajapata taarifa kuwepo kwa tukio hilo.

No comments: