Saturday, April 06, 2013

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA PADRE MUSHI AFIKISHWA KORTINI

,,



Mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evarist Mushi wa kanisa la Roman Katoliki jimbo la Zanzibar, Omar Mussa Makame (35), jana amefikishwa mahakamani kusomewa shitaka lake.
 
Mtuhumiwa huyo ambaye aliwahi kuwa mgombea wa nafasi ya Uwakilishi katika jimbo la Raha Leo kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), anatuhumiwa kufanya mauaji hayo Febuari 17, mwaka huu.
 
Alifikishwa mahakamani majira ya saa 5 asubuhi na kusomewa mashtaka na Mwanasheria wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Abdallah Issa Mgongo, akisaidiwa na Mohamed Saleh Iddi.
 
Alidai kuwa Febuari 17, mwaka huu majira ya saa 12:59 asubuhi, mshitakiwa anatuhumiwa kumuua Padri Mushi kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha sheria namba ya 6 ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004.
 
“Mshtakiwa anatuhumiwa kumuua Padri Mushi, katika eneo la Beitrasi, majira ya saa 12:59 kinyume na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya Zanzibar,” alisema Mgongo.
 
Hata hivyo, Mgongo alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu.
 
Kwa upande wake, baada ya kusomewa shtaka hilo, Omar Mussa Makame alikana kosa hilo na anatetewa na Wakili Abdallah Juma Mohamed akisaidiwa na Rajab Abdallah Rajab.
 
Kabla ya mtuhumiwa kusomewa shtaka lake, Wakili Abdallah Juma alioomba mahakama itoe mwongozo kufuatia ombi alilofungua Mahakama Kuu, akitaka Naibu Mkurugenzi wa upelelezi na makosa ya jinai Zanzibar, aitwe mahakamani kueleza kwanini mteja wake hakufikishwa mahakamani tangu alipokamatwa Machi 17, mwaka huu, kinyume na sheria.
 
Alisema ombi hilo tayari limepangiwa kusikilizwa Aprili 8, mwaka huu, na ana wasiwasi kitendo cha mshtakiwa kufikishwa mahakamani na kusomewa shtaka lake kunaweza kuathiri mwenendo mzima wa ombi hilo na kuomba mahakama kuondoa shauri hilo la mteja wake kusomewa mashataka hadi hapo ombi lake litakapotolewa maamuzi.
 
“Ombi letu kwako mheshimiwa, naomba mahakama kuondoa shauri la kumsomea shtaka mtuhumiwa, ili kutoa nafasi ya kusikiliza ombi tulilolifungua mbele ya mahakama yako,” alisema Abdallah Juma.
 
Hata hivyo, mwendesha mashtaka wa serikali, Mgongo, alisema ombi hilo halina uhusiano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, na wala haijataarifiwa kuhusu kufunguliwa kwa ombi la kuhusiana na kesi hiyo.
 
“Ofisi ya DPP haijataarifiwa kuhusu ombi hilo, na haina taarifa yoyote, na kwa mujibu wa katiba, Mkurugenzi wa Mashtaka ndiye mwenye mamlaka ya kufungua kesi na ndicho kilichotuleta hapa,” alisema Mgongo.
 
Aidha alisema ombi lililofunguliwa mahakamani haliathiri shauri liliopo mbele na kuitaka mahakama kuzingatia kilicholetwa mbele yake, nacho ni kumsomea shtaka mtuhumiwa wa mauaji hayo.
 
Kwa upande wake, Jaji Mkusa baada ya kusikiliza pande hizo mbili, alisema kwamba ombi lililofunguliwa katika mahakama na wakili wa mtuhumiwa, la kuhoji kwanini hakufikishwa mahakamani ndani ya saa 24, bado haliathiri hatua ya kumsomea shtaka mtuhumiwa.
Jaji Mkusa alisema ombi lililofunguliwa litaendelea kusikilizwa kama lilivyopangwa, na mahakama, kazi yake kubwa ni kutafsiri sheria na kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria.
 
Hata hivyo, Jaji Mkusa alitoa angalizo kwa vyombo vya habari kuwa makini wanaporipoti kesi ya mauaji kama hiyo, ili kuepuka kuvaa koti la mahakama la kumhukumu mtu kabla ya kuhukumiwa na mahakama ambayo ndio yenye jukumu hilo kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Jaji Mkusa ameiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 18, mwaka huu.
Padri Evarist Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akienda kuongoza misa ya Jumapili, katika kanisa la Mtakatifu Theresia lililopo eneo la Beitrasi, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

No comments: