Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alisema tukio hilo
lilitokea jana saa 3:30 katika kijiji cha Misima wakati wakielekea
katika kijiji cha Nzundu kwenye zoezi la upandaji miti lililokuwa
likifanyika kiwilaya kijijini hapo.
Aliwataja waliofariki papo hapo baada ya ajali kutokea kuwa ni
Hamis Bwanga ambaye ni mwandishi wa gazeti la Uhuru na Mzalendo na Ofisa
Uhamiaji Wilaya ya Handeni, Mariamu Hassani.
Rweyemamu alisema mwandishi Sonyo Mwankale
(Hussein Semdoe), alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya
Handeni akipatiwa matibabu.
Katika ajali hiyo, Mwankale ambaye alijeruhiwa vibaya sehemu za
kichwani, baada ya kupelekwa hospitalini hapo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni
alimuomba helkopita Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Said Mwema,
kuwachukua majeruhi hao, lakini kabla haijafika mwandishi huyo akafariki
dunia.
Wengine waliyojeruhiwa katika ajali hiyo na kulazwa kwenye
hospitali hiyo ni Mshauri wa Mgambo Wilaya, Athanas Paulo, Ofisa Misitu
Wilaya, Natorin Mloe na dereva wa gari hilo lenye namba za usajili STK
4673, Mlawa Makata.
Habari zilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni gari hiyo ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Handeni, kupasuka gurudumu la nyuma na
kuacha njia kisha kupinduka. Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakuwamo katika
gari hiyo.
Wakizungumzia ajali hiyo, kwenye eneo la tukio, mashuhuda hao
alisema watu hao walipoteza maisha muda mfupi mara baada ya tukio hilo
na kwamba wananchi waliyojitokeza kutoa msaada walishuhudia hali za
majeruhi hao zikiwa mbaya.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Rweyemamu akizungumzia tukio hilo
alisema kifo cha Afisa Uhamiaji huyo ni pigo kwa wilayani kwani ni hivi
karibuni alisaidia kukamatwa kwa wahamiaji haramu 74.
Ofisa misitu Wilaya ya Handeni, Mloe akizungumzia jinsi ajali hiyo
ilivyotokea akiwa katika hospitali ya Wilaya Handeni alikolazwa, alisema
wakiwa safarini mbele alijitokeza mwendesha pikipiki (bodaboda) akitaka
kujaribu kuwapita.
Alisema dereva wa gari lililobeba alimkwepa dereva wa bodaboda na
kusababisha gari kuyumba na kusababisha kupinduka upande wa pili wa
barabara na hivyo kusababisha kifo cha Afisa Uhamiaji na mwandishi wa
gazeti la Uhuru papo hapo.
No comments:
Post a Comment