Watu wawili wameuawa katika matukio tofauti
mkoani Mbeya wakati wa sikuu ya Krismas likiwamo tukio la kijana mmoja kumuua
kaka yake kwa kumchoma kisu.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alisema kuwa katika tukio la kwanza
lililotokea majira ya saa 2:00 asubuhi katika maeneo ya Sae Jijini Mbeya, mtu
mmoja ambaye bado hajafahamika, aliuawa na wanachi wenye hasira baada ya
kumtuhumu kuwa ni mwizi.
Alisema kuwa mtu aliyeuawa ni kijana
anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 20 na 25 ambaye alishambuliwa kwa
marungu na mapanga hadi mauti yalipomfika.
Kamanda Diwani alisema kuwa
baada ya mauaji hayo, watu waliokuwa wakimshambulia walitoweka na kuwa hadi sasa
Jeshi la Polisi halijagundua marehemu alitaka kuiba nini wala mahali
alipotuhumiwa kuiba.
Katika tukio la pili lililotokea wilayani Rungwe,
Kamanda Diwani alisema kuwa kijana Itamu Mwakagenda (23) aliuawa kwa kuchomwa
kisu kifuani na ndugu yake aitwaye Nebo Daudi maarufu kwa jina la Isalikila
wakati wakigombea panga.
Kamanda Diwani alisema kuwa majira ya saa 12:00
asubuhi wakati watu wakijiandaa kwenda kanisani, kuliibuka ugomvi miongoni mwa
wanandugu hao kila mmoja akihitaji panga ili alitumie kwa shughuli
zake.
Alisema ugomvi huo ulisababisha Nebo mwenye umri wa miaka 21
kuchukua kisu alichokitumia kumchoma kifuani kaka yake na kumsababishia kifo
papo hapo.
Alisema baada ya mauaji hayo Nebo alitoroka na kuwa hadi sasa
Jeshi la Polisi linaendelea na msako dhidi yake ili afikishwe kwenye vyombo vya
sheria.
Aidha, Kamanda Diwani alisema kuwa mbali na matukio hayo ya
mauaji, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu 16 waliokamatwa kwa
tuhuma mbalimbali zikiwamo za kukutwa na bangi na unywaji wa pombe haramu ya
gongo.
No comments:
Post a Comment