Msanii nyota wa filamu na muziki wa injili, Ummy Wenceslaus 'Dokii' sasa
ameamua kutumia umaarufu wake kupunguza ajali zitokanazo na pikipiki
kupitia taasisi yake ya Tanzania Women Entertaiment ambapo mwishoni mwa
wiki aligawa zawadi kadhaa katika tamasha alilowaandalia madereva wa
chombo hicho liitwalo 'Dokii Boda Kibajaji Festival'.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa tamasha hilo lililofanyika kwenye
viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Dokii
aliyewahi kung'ara katika tamthilia mbalimbali zilizokuwa zikirushwa
kupitia kituo cha luninga cha ITV, alisema kuwa nia yake ni kutumia
uzoefu wake katika sanaa ili kuwahamasisha madereva wa bodaboda kuzijua
sheria na kuzifuata.
"Ajali nyingi zinazotokea barabarani hivi sasa zimekuwa zikiwahusisha
madereva wa bodaboda. Nimeamua kushirikiana na wadau ili kuwahamasisha
wajifunze sheria za barabarani na kuzizingatia ili kuwapunguzia matukio
ya ajali zinazoepukika," alisema Dokii.
Katika tamasha hilo ambalo lilihusisha pia shindano la kumsaka dereva
bora wa bodaboda, washindi kutoka kila wilaya jijini Dar es Salaam
walikuwa ni madereva Ismail Mohamed wa Ilala, Amir Mlamu (Temeke) na
Kaiwanga Rajab wa Kinondoni. Kila mmoja miongoni mwa washindi hao
alipata zawadi ya pikipiki aina ya Fekon na waliozikabidhi walikuwa ni
Dokii na msanii nyota wa bongofleva, Juma Nature.
No comments:
Post a Comment