Jana Jiji la Mwanza kwa takribani saa mbili lilitikiswa na milio ya
mabomu ya kutoa machozi na risasi za moto wakati askari wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU) walipokuwa wakiwatawanya madereva wa pikipiki za
abiria maarufu kama bodaboda.
Madereva hao walikuwa wakifanya vurugu kupinga hatua ya askari wa Kikosi
cha Usalama Barabarani kukamata pikipiki zao kwa madai kuwa wanakiuka
sheria na taratibu.
Operesheni ya kukamata pikipiki hizo ilianza juzi, lakini jana madereva
hao wanaodai kuwa wanaonewa, walikosa uvumilivu na kutumia nguvu kupinga
kwa kujikusanya barabarani
wakitaka kuwadhuru askari wa usalama barabarani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, aliwaambia waandishi wa
habari jijini hapa jana kuwa tukio hilo lilitokea saa 3:30 asubuhi
katika eneo la Misheni kwenye barabara ya kuelekea Uwanja wa Ndege.
Alisema kwamba baadhi ya askari wake walikuwa katika operesheni maalum
ya kukamata madereva wa vyombo vya usafiri wasiozingatia sheria za
usalama barabarani.
Kwa mujibu wa Kamanda Mangu, operesheni hiyo ilianza tangu juzi na kwa
siku ya kwanza ilifanyika kwa ufanisi mkubwa pasipo vikwazo vyovyote.
Hata hivyo, alisema jana askari walijielekeza zaidi katika kuwakamata
madereva ambao wanaendesha bodaboda pasipokuwa na leseni au kofia ngumu
(helmet) na wale wanaopakia abiria zaidi ya mmoja maarufu kama
mishikaki.
Aidha, alisema kwamba operesheni hiyo kwa jana ililenga pia madereva wa
bodaboda wenye tabia ya kuendesha upande wa kushoto mwa barabara
wanakopita waenda kwa miguu na hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara.
“Ni kweli kwamba tumekuwa na operesheni maalum ya kukamata madereva
wanaovunja sheria za usalama barabarani na leo (jana) tulijielekeza
zaidi kwa madereva wa bodaboda, na tayari jumla ya pikipiki 26 zilikuwa
zimekamatwa,” alisema.
Aliongeza kwamba kati ya pikipiki 26 zilizokuwa zimekamatwa, madereva 10
waliopatikana na makosa walikubali kulipa faini na kuachiwa.
Hata hivyo, alisema wakati zikiwa zimebaki pikipiki 16, ghafla lilizuka
kundi kubwa la madereva wenye pikipiki na kuwazunguka askari, kupiga
kelele za honi na kufunga barabara hali iliyosababisha usumbufu kwa
watumiaji wengine wa barabara na shughuli kusimama kwa takribani saa
mbili kutokana na vurugu hizo.
Kadhia hiyo iliwakumba wakazi wanaoishi maeneo ya barabara ya Uwanja wa
Ndege kuanzia Kliniki, Nela, Misheni hadi Ghana baada ya madereva hao
kuifunga.
Kufuatia hali hiyo, Kamanda Mangu alisema kwamba askari waliokuwapo
walilazimika kuomba msaada na walitumwa FFU ambao baada ya kufika wenye
pikipiki walianza kuwarushia mawe, ndipo nao wakawatawanya kwa kurusha
mabomu ya kutoa machozi.
Hata hivyo, ushahidi wa picha ya video umemuonyesha mmoja wa askari hao
wa FFU akirusha hewani risasi kadhaa za moto na kusababisha hofu kubwa
miongoni mwa wapita njia na wananchi wanaofanya shughuli zao eneo la
Misheni.
Kutokana na vurugu hizo, Kamanda huyo alisema kuwa watu wanane walitiwa
mbaroni pamoja na pikipiki 13 ambazo wahusika walizitelekeza na kukimbia
wakati wakitawanywa na askari wa FFU. Hata hivyo, alisema hakuna mtu
aliyepata majeraha makubwa, isipokuwa mikwaruzo midogo kwa askari wake,
hali ambayo alisema ni ya kawaida katika zoezi kama hilo.
Pamoja na kuzuka kwa ghasia hizo, alisema kuwa Jeshi la Polisi
litaendelea na operesheni hiyo kwa wiki nzima ili kuhakikisha madereva
wanatii sheria za usalama barabarani kwa lengo la kupunguza ajali
zinazoepukika.
No comments:
Post a Comment