Wednesday, January 23, 2013

LULU AANZA KUTAFUTA DHAMANA

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itaanza kusikiliza ombi la dhamana ya msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael (pichani) maarufu kama Lulu  Januari 25 mwaka huu.

Msanii huyo anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven Kanumba; kesi yenye jalada Na. 125/2012.

Ombi hilo la dhamana litaanza kusikilizwa kwa Jaji Zainabu Mruke mahakamani hapo na lilitoka kwa mawakili Lulu ambao ni Peter Kibatala, Kennedy Fungamtama na Massawe Fulgence. Kesi hiyo ya kuua bila kukusudia bado haijapangwa tarehe ya kusikilizwa.

Kulingana na hati ya ombi hilo la dhamana ya Lulu, mawakili wameonyesha kwamba wanawasilisha ombi hilo chini ya kifungu 148 (1) na (2) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Mawakili wa Lulu walidai kuwa kosa analotuhumiwa mshtakiwa linadhaminika ikiwa atatimiza masharti ya dhamana yatakayotolewa na hakimu.

Kulingana na hati ya mashitaka, Lulu anatuhumiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, 2012 katika eneo la Sinza Vatican, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
 

No comments: