Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, ametimuliwa kwenye kikao cha
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa
madai kwamba ana maslahi ya upande mmoja katika mgogoro uliotokea
bungeni juzi wakati Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alipokuwa
akijibu hoja ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Taarifa za uhakika zilizopatikana bungeni jana zilieleza kwamba Mdee
ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, alizuiwa kuhudhuria kikao kilichojadili
sakata hilo kwa kuwa alikuwa akishabikia vurugu bungeni.
Taarifa zaidi zimedai kwamba kumeibuka mvutano kuhusu kanuni iliyotumika
kumruhusu Waziri Maghembe kutumia nusu saa kujibu hoja ya Mnyika wakati
alipaswa kutumia dakika 15 kama wachangiaji wengine.
Jana Mdee alithibitishia NIPASHE kuwa alizuiwa kuhudhuria kikao cha
kamati hiyo kwa maelezo kuwa ana maslahi na upande wa kambi ya upinzani
juu ya suala la mgogoro wa hoja ya Mnyika ambayo ilipokwa na serikali
juzi na kuiua.
Mdee alielezwa kuwa alikuwa bungeni siku hiyo na alishiriki katika
kadhia iliyosababisha Bunge kuahirishwa kabla ya muda wake baada ya
wabunge wote wa Chadema na NCCR-Mageuzi kusimama kwa muda mrefu na
kuzuia shughuli za Bunge kuelendelea wakipinga kitendo cha kuvunjwa kwa
kanuni za Bunge kwa kuipa nafasi serikali uondoa hoja binafsi ya Mnyika
juu ya upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika jiji la
Dar es Salaam.
Kamati ya Maadili imepewa jukumu la kuchunguza chanzo cha vurugu hizo
kwa kuwahoji wabunge waliohusika na kadhia ya Jumatatu jioni ili kutoa
mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa dhidi yao.
WAJUMBE WA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE
Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi (Mwenyekiti); Christopher Ole Sendeka;
Rashid Ali Abdallah, Dk. Maua Daftari; John Chiligati; Dk. Christina
Ishengoma; Riziki Omar Juma; David Kafulila; Vita Kawawa; Philemon
Ndesamburo; Augustino Masele, Said Arfi; Augustine Mrema; Cynthia Ngoye;
Halima Mdee na Gosbert Blandes.
Hata hivyo, Chadema imewaelekeza wabunge wake wote kutoitikia wito wa
kamati hiyo hadi hapo Spika wa Bunge, Anne Makinda, atakapotoa uamuzi wa
rufaa 10 ambazo wabunge hao wamekata kwake, lakini amezikalia tangu
mwaka 2011.
Pia Chadema kimetishia kuwasilisha hoja ya kumng'oa madarakani Spika
Makinda na Naibu Spika, Job Ndugai, kwa madai ya kukiuka kanuni za Bunge
kwa kutotenda haki kwa pande zote, hasa kambi ya upinzani, kwa maana
hiyo wamepoteza sifa za kuongoza muhimili huo.
WABUNGE HAWAJAHOJIWA
Wakati huo huo, Kamati hiyo bado haijawahoji wabunge wanaodaiwa kufanya fujo ndani ya Bunge.
Taarifa zilizoifikia NIPASHE, zilieleza kwamba hakuna hata mbunge mmoja ambaye amepewa samansi ya kuitwa kwenye kamati hiyo.
Katika hatua nyingine, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu
Lissu, amesema kitendo cha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumtuhumu kuwa
ni mropokaji namba moja bungeni ni kwa sababu ya chuki na upendeleo
dhidi ya wabunge wa upinzani.
Akizungumza na NIPASHE jana Lissu alisema siyo kweli kwamba amekuwa ni
mropokaji bungeni kama Spika Makinda alivyomtuhumu na kwamba amekuwa
akifuata kanuni zinazotakiwa kwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa
kuisimamia na kuishauri serikali.
Alisema yeye ni miongoni mwa wabunge wachache ambao wanazifahamu kanuni za Bunge, Katiba ya nchi na sheria mbalimbali.
“Kuniita mropokaji ni kunifananisha na baadhi ya wabunge wa CCM ambao
hawajui sheria wala wajibu wa Bunge…wanadhani kazi ya mbunge ni
kuikingia kifua serikali na kuitetea, wamesahau kwamba wajibu wao ni
kuishauri na kusimamia, " alisema.
Lissu alisema kamwe hawezi kuogopa kuisimamia serikali kama Katiba
inavyomtaka na hawezi kuitetea pale inaposhindwa kuwahudumia wananchi
kwa ufanisi.
KAMATI KUCHUNGUZA MTAALA
Katika hatua nyingine, Bunge limeunda kamati ya wabunge sita kuchunguza
mitaala ya shule ya awali, msingi na sekondari iliyowasilishwa bungeni
na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ili
kubaini kama ina upungufu au la.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James
Mbatia, wiki iliyopita, kuitaka serikali kuonyesha mitaala hiyo.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema baada ya kipindi cha maswali
na majibu bungeni jana kuwa amekabidhiwa mitaala hiyo na ameunda kamati
hiyo ili ikajiridhishe juu ya jambo hilo.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni Mbunge wa Kibiti (CCM) Abdul Jabiri
Marombwa; Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahya Kassim Issa na Mbunge wa Karatu
(Chadema), Israel Natse.
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Benardetha Mushashu; Mbunge wa
Viti Maalum (CCM) Margaret Sitta na Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa
Suleiman Khalifa.
Ndugai alisema wengine watakaoingia kwenye kamati hiyo kuwa ni Mbatia,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Kamishina wa Elimu, Mwanasheria wa
Wizara na wataalamu wengine wa elimu.
Hata hivyo, Ndugai aliitaka kamati hiyo kufanya kazi yake jana na
ifikapo leo iwe imekuja na majibu juu ya suala hilo. Wiki iliyopita,
Mbatia aliwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu udhaifu katika sekta ya
elimu na kutaka mfumo unaosimamia elimu nchini ufumuliwe.
Alitaja udhaifu uliopo katika sekta ya elimu kuwa ni pamoja na
kutokuwapo sera ya pamoja kuhusu elimu, matatizo ya mitaala na utungaji
wa vitabu vya kufundishia shuleni.
Hoja ya Mbatia ilizua mjadala mrefu bungeni kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mitaala, sera na mihutasari ya elimu.
Baadhi ya wabunge walitaka kamati ya Bunge na wengine walitaka iundwe tume huru ya kufuatilia suala hilo.
Mjadala huo uliendelea kwa Dk. Kawambwa kutetea mfumo wa elimu uliopo na
mtaala, kabla ya wabunge kuchangia na Mbatia kuhitimisha hoja yake.
Akiwasilisha hoja yake, Mbatia aling’ang’ania kupatiwa mitaala hiyo,
jambo ambalo Dk. Kawambwa alijibu kuwa ilikuwapo ingawa hakuwa nayo
bungeni.
Baada ya majibu ya Dk. Kawambwa, Mbatia aliomba hoja yake iahirishwe hadi mitaala itakapowasilishwa bungeni.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi, alisimama bungeni na kuhoji: “Katika kikao kilichopita,
hata katika hansard, tulisema mtaala utawasilishwa katika kikao hiki,
sasa wasiwasi wa mbunge (Mbatia) ni nini? Hata siku ya mwisho ya Bunge
tutaleta.”
Baada ya kauli hiyo, Ndugai alipiga kura kwa kuuliza wanaotaka hoja
imalizike na baada ya majibu, aliruhusu Mbunge wa Nzega (CCM), Dk.
Hamisi Kigwangalla, kuwasilisha hoja binafsi kuhusu ajira kwa vijana na
kilimo.
Hata hivyo, baada ya kumruhusu Dk. Kigwangalla, wabunge wa upinzani
walitoka nje ya Bunge na kufanya mkutano wa dharura uliochukua dakika 38
katika ukumbi wa Pius Msekwa.
HAKIELIMU YAIBANA SERIKALI
Katika hatua nyingine, serikali imetakiwa kuacha ubabe wa kupangua hoja
zinazotolewa na watalaamu wa masuala ya elimu, ambao wanafanya utafiti
na kuainisha upungufu uliopo katika sekta hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na wanaharakati wa masuala ya elimu, ambao
wameunga mkono hoja iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Mbatia,
aliyetaka Bunge lichunguze udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu linalojishughulisha na
masuala ya elimu, Elizabeth Misokia, aliwaaambia waandishi wa habari
ofisini kwake jana kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote na kwamba,
kitendo cha serikali kukosoa tafiti za watalaamu na kuzitupa, hakilengi
kuijenga nchi na kuinua kiwango cha elimu nchini.
“Serikali isitumie nguvu nyingi kukosoa tafiti mbalimbali zinazofanywa
na watalaamu kuhusu elimu, badala yake izifanyie kazi ili kuziboresha,”
alisema Misokia.
Alisema sera ya elimu ya mwaka 1995 haieleweki inasema nini kuhusu elimu
na kwamba, hata mitaala ya kufundishia nayo haileweki kwa walimu
wanaoitumia kufundishia.
Misokia alisema sekta ya elimu nchini inakabiliwa na matatizo mengi,
ukiwamo uhaba wa walimu, walimu kukata tamaa kutokana na serikali
kuwapuuza, kushindwa kuwalipa madai yao ya siku nyingi pamoja na kufanya
kazi katika mazingira magumu.
Matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu, ni pamoja na wakaguzi
kushindwa kufika katika shule mbalimbali kwa ajili ya kuzikagua.
Alisema kati ya mwaka 2000 hadi 2002 elimu ya shule ya msingi
ilipanuliwa, lakini hakuna juhudi zozote za kuwapo sera moja ya elimu
itakayoisimamia kikamilifu.
Aliomba serikali kutengeneza kwanza sera yenye nguvu kuhusu elimu kabla
ya kuanza kuandaa mitaala inayofanana nchini kote ili kuhakikisha
wanafunzi wanapata elimu inayofanana na iliyo bora.
No comments:
Post a Comment