Thursday, February 07, 2013
WASANII WAPIGWA MARUFUKU KUVAA KOMBATI ZA JESHI
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imewapiga marufuku wasanii wote nchini kuvaa mavazi yanayofanana na sare za jeshi la wananchi.
Onyo hilo lilitolewa jana bungeni na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha alipokuwa akijibu swali la nyongeza na Mbunge wa Viti Maalum, Maryam Salum Msabaha.
Msabaha alisema sare hizo za jeshi la polisi zimekuwa zikiuzwa katika maduka ya nguo mbalimbali na kusababisha hata wasanii kuzitumia katika kazi zao.
“Sare hizi zimekuwa zinazagaa zagaa hata wasanii siku hizi wanazitumia katika kazi zao za muziki… je, serikali hailioni hili nalo kuwa ni tatizo kwenye kazi zetu?” alihoji mbunge huyo.
Akijibu swali hilo, Nahodha alisema kuna wasanii ambao wamekuwa wakitumia sare ambazo zinafanana na sare za kijeshi na kudai kuwa hawatakiwi kuzitumia.
“Najua wapo wasanii ambao wanatumia sare hizo…narudia kusema kuwa ni marufuku kwa watu wasiohusika kuendelea kutumia mavazi yanayofanana na mavazi ya kijeshi,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kuwasaka wale wote wanaotumia mavazi hayo na iwapo itaridhika kuwa wana mavazi ambayo yanafanana na sare za kijeshi hawatasita kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
“Tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali na bado napenda kusema tutaendelea na zoezi hili,” alisema
Awali katika swali katika swali lake la msingi, mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuboresha sare za jeshi la wananchi ili kudhibiti wimbi la uhalifu kwa kuvaa mavazi hayo.
Akijibu swali hilo, Nahodha alisema matumizi ya sare za jeshi yanayofanywa na wahalifu hayatokani na sare hizo kukosa ubora bali yanatokana na namna sare hizo zinavyodhibitiwa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment