.
Jeshi la Polisi Zanzibar limeanza kuwahoji watu tisa kuhusiana na mauaji
ya Padri Evaristus Mushi, wa Kanisa Katoliki Zanzibar, aliyeuawa kwa
kupigwa risasi Jumapili iliyopita na watu wasiojulikana.
Padri Mushi alizikwa juzi katika makaburi ya mapadri eneo la Kitope Mkoa Kaskazini Unguja.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Yussuf Ilembo,
alisema watu hao walikamatwa na kikosi kazi kilichoundwa kwa kuwahusisha
maafisa wa upelelezi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
“Watu tisa tumewakamata na kuwahoji kama hatua ya kwanza kuwatafuta na
kuwakamata watu waliohusika na mauaji, Tumefikia hatua kubwa ya kuwasaka
watu hao,” alisema Ilembo.
Hata hivyo, alisema ni mapema kutaja majina na mitaa wanayoishi kutokana
na kuhofia kuvuruga uchunguzi na kuongeza kuwa timu ya wapelelezi
inaendelea na kazi yake ikiwamo kukusanya taarifa za kusaidia kuwapata
wahalifu hao.
Alisema wananchi wanapaswa kulisaidia Jeshi la Polisi kutoa taarifa za
siri kuhusu watu wanaowatilia shaka kuhusiana na vitendo vya hujuma
dhidi ya viongozi wa dini.
Kuhusu watu watatu kudaiwa wamekamatwa huko Mombasa, Kenya, Ilembo
alisema taarifa hizo hazina ukweli ingawa wanaendelea na uchunguzi kwa
kushirikiana na vyombo vya ndani na nje.
MAKACHERO WA NJE KUWASILI
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi wa Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud
Mohamed, alisema mpango wa kuwaleta makachero wa kimataifa umefikia
hatua nzuri na wakati wowote watawasili Zanzibar.
Aboud alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais
Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kuvitaka
vikosi vya ulinzi kushirikiana na kukaribisha vikosi vya nchi rafiki
kufanikisha msako huo.
“Tunatafuta shina na mizizi ya uahalifu huu mahali popote ulipo, tuko
tayari kumkamata mtu yeyote bila ya kujali wadhifa, cheo au jina lake,”
alisema na kuongeza:
“Ndiyo maana tumeamua kukaribisha watu wenye utaalam mkubwa katika
masuala ya upelelezi na lengo letui ni kukusanya ushahidi wa kutosha.”
Alisema tayari vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)
vimeingia kazini kwa kushirikiana na vya Muungano na Jeshi la Polisi na
kuimarisha doria maalum hasa katika maeneo nyeti ya kuingia na kutoka.
Waziri Aboud aliongeza kuwa Rais Shein ameiagiza timu ya upelelezi kumpatia taarifa ya maendeleo kila baada ya muda maalum.
ASKOFU LEBULU ATOA KAULI KALI
Akofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu,
amesema, Wakristu wanao uwezo wa kulipiza kisasi dhidi ya mauaji ya
viongozi wao yanayofanywa na aliowaita mashetani na mawakala wao na
wangekuwa na haki ya kufanya hivyo, lakini, Kristo, anawataka wasilipize
kisasi ili kumpa shetani ushindi.
“Sisi siyo wapumbavu na kwamba hatuwezi kufanya chochote…tunavutwa tu na
huruma ya Mwenyezi Mungu tukae kimya, lakini hakuna mwanadamu yeyote
anayeweza kuvumilia hili. Katika mazingira halisi ya kibinadamu, hakuna
hata mmoja ambaye atafurahia mauaji haya isipokuwa shetani na mawakala
wake,” alisema.
Askofu huyo aliwataka Wakristu na waumini wa dini nyingine wenye mapenzi
mema, wasitawaliwe na hasira, chuki wala mioyo ya kulipa kisasi kwa
sababu Yesu Kristu amewataka wasifanye hivyo, ingawa uwezo wa kufanya
hivyo wanao na haki ingekuwa upande wao.
Alisema hayo katika mahubiri yake ya Misa ya Wafu ya kumwombea marehemu Padri Mushi.
Katika misa hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Theresa wa
Mtoto Yesu jijini hapa jana na kuhudhuriwa na mamia ya waumini wa dini
hiyo na wa madhehebu mengine, Askofu Mkuu Lebulu, alisema: “Tusilipe
kisasi, bali tushinde kwa yaliyo mema.”
“Kama Mungu yupo nasi na yupo upande wetu, hata kama kwa mabavu na
bunduki, hakuna wa kututenganisha na upendo wa Kristu. Je, ni dhiki,
njaa, uchi, hatari au upanga,” alihoji na kuongeza: “Lakini haya yote
tunayashinda kwa Jina la Yesu na yeye anatupenda na hakuna chochote
kitakachotutenga na upendo wa Kristu.”
Akizungumzia mauaji hayo, alisema wanaamini ukweli wa mambo hayo
yatajulikana maana hakuna kinachotendeka kwa siri ambacho hudumu hivyo
hivyo bila kujulikana.
Askofu Mkuu Lebulu, alisema Watanzania wanalia kama watoto yatima kwa
kukosa baba au wazazi na akaelezea kushangazwa kwake kuhusu kauli za
vitisho, matusi na kuleta hofu zilizokuwa zikisambazwa na baadhi ya watu
kwa njia za CD, kanda na ujumbe wa simu, huku vyombo vya usalama
vikitazama tu, halafu baadaye wanalalamika maadili yameshuka.
“Unashangaa vyombo vya usalama vinaangalia tu, zipo kanda nyingi za
matusi na vitisho dhidi ya waumini wa dini nyingine…vipo wapi vyombo vya
usalama kama wengine wanauawa namna hii. Mungu awaguse mioyo yao na
wabadilike na kumgeukia Mungu.
“Mambo hayo watu wa usalama wamezembea, tangu awali kulikuwapo na
viashiria vingi sana vya kuwapo hofu ya mauaji, lakini kwa nini
hawashughulikiwi,” alihoji na kuongeza, “pengine hapa kuna siri
imejificha.”
Alilaani pia mauaji ya Mchungaji Mathayo Kachila (45), wa Kanisa la
Pentekoste la Assemblies of God, mkoani Geita, uchomaji moto wa makanisa
na tukio la kumwagiwa tindikali kwa Sheikh huko Zanzibar kunakofanywa
na baadhi ya watu kwa malengo wanayoyajua wao wenyewe na akasema vitendo
hivyo havisaidii kuleta amani ya taifa.
No comments:
Post a Comment