Kati ya waliofariki, mmoja ametambuliwa kwa jina la Sabrina Is-haka
(11), ambaye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali
ya Wilaya ya Temeke.
Mwingine mwanaume, ambaye jina lake halijafahamika, anayekadiriwa
kuwa na umri wa kati ya miaka 30-31, alifariki dunia papo hapo katika
eneo la ajali.
Mkuu wa askari polisi wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani Mkoa wa
Temeke, Prackson Rugazia, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Pia Mwangalizi Mkuu wa jana wa Hospitali hiyo, Amosi Kaberege,
alithibitisha hospitali yake kupokea majeruhi hao pamoja na miili ya
watu waliofariki kuhifadhiwa hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa Kaberege, marehemu Sabrina, ambaye alikuwa na pacha
mwenzake katika gari lililopata ajali, alifariki dunia kutokana na
kutokwa na damu nyingi baada ya kukatika mguu.
Aidha, kati ya waliojeruhiwa, 42, akiwamo pacha wa marehemu Sabrina, walitibiwa katika hospitali hiyo na kuruhusiwa.
Hata hivyo, majeruhi wawili kati yao, walihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa Rugazia, ajali ya kwanza ilitokea katika Barabara ya
Kilwa, eneo la Msikitini, Mtoni Mtongani, saa 12.30 asubuhi jana,
ikihusisha daladala mbili aina ya Toyota DCM linalofanya safari zake
Mwenge-Mbagala na Eicher la Mbagala-Kivukoni, yaliyogongana.
Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya daladala aina ya Eicher
lililokuwa likitokea Kivukoni kuacha njia na kwenda upande wa pili wa
barabara na kuligonga daladala aina ya Toyota DCM lililokuwa likitokea
Mbagala kwenda Mwenge.
Rugazia alisema dereva wa Toyota DCM, ambaye ni mmoja wa majeruhi
alijisalimisha, lakini yule wa Eicher alikimbia baada ya ajali hiyo na
kwamba, polisi wanaendelea kumsaka.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ajali hiyo ilisababishwa
na usukani wa Eicher kugoma kufanya kazi, hali iliyomfanya dereva wake
kushindwa kulimudu gari hilo.
Aidha, kwa mujibu wa Kaberege, jana pia walipokea hospitalini hapo
watu 11 waliojeruhiwa katika ajali iliyohusisha daladala aina Toyota
Hiace iliyogongana na Fuso.
Alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kwa Sokota, wilayani
humo, majira ya saa 4 asubuhi. Hata hivyo, alisema watu hao walitibiwa
na kuruhusiwa.
No comments:
Post a Comment