Friday, February 08, 2013

MV VICTORIA YANUSURIKA KUTEKETEA KWA MOTO



 Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ernest Mangu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini alisema jitihada za wafanyakazi wa meli hiyo pamoja na kikosi cha Zimamoto zilifanikisha kuudhibiti moto huo kabla haujasababisha madhara makubwa.

Alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 9:00 alasiri katika bandari ya Mwanza Kaskazini wakati meli hiyo ikipakiwa mizigo tayari kwa safari ya kuelekea Bukoba ambayo kwa kawaida huanza saa3: 00 usiku.

Kwa mujibu wa Kamanda Mangu, wakati meli hiyo ikiendelea kupakiwa mizigo, mafundi waashi pia walikuwa wakiendelea na kazi ya kuchomelea sehemu zilizokuwa zimetoboka.
Alibainisha kuwa cheche za moto ziliruka na kupenya hadi chini ya meli inakokaa mizigo na kusababisha kuzuka kwa moto ambao uliunguza jumla ya mito 400 ya makochi ambayo hata hivyo thamani yake haikukujulikana mara moja.

“Taarifa tulizozipokea ni kwamba hakuna uharibifu mkubwa uliosababishwa na moto huo isipokuwa mito 400 ya makochi iliyokuwa ikisafirishwa kama mizigo ndiyo iliyoteketea kwa moto, lakini thamani yake bado haijafahamika tunaendelea kuwasiliana na wahusika ili watueleze,” alisema.

Hata hivyo, alisema aliwasiliana na Kampuni ya Huduma za Meli (MSC) na wamemthibitishia kuwa meli hiyo ilitarajiwa kuendelea na safari ya kwenda Bukoba kwa vile hakuna hitilafu yoyote ya kiufundi iliyotokea.

Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) mkoani Mwanza, Japhet Loismeye, alisema ukaguzi uliofanywa umeonesha meli hiyo haikupata matatizo yoyote ya kiufundi hivyo inaruhusiwa kuendelea na safari baada ya taratibu zingine kukamilika.

No comments: