Monday, February 18, 2013
PADRE AUAWA ZANZIBAR
Padri Evaristus Mushi, wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph- Shangani Mjini Magharibi, visiwani Zanzibar, ameuawa kikatili kwa kupigwa risasi tatu kichwani huku wauaji wake wakitoroka bila kukamatwa.
Mauaji haya ni mfululizo wa hujuma dhidi ya viongozi wa dini visiwani Zanzibar na linatokea zaidi ya mwezi mmoja baada ya Padri Ambrose Mkenda, kujeruhiwa kwa kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi na watu wasiofahamika mwishoni mwa Desemba, mwaka jana, hadi leo waliotekeleza unyama huo hawajakamatwa.
Jana Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, aliitisha mkutano wa ghafla na waandishi wa habari Makao Makuu ya Polisi kutoa taarifa za mauaji ya Padri Mushi, mbali ya kuthibitisha unyama huo, alisema aliuawa na watu wasiofahamika majira ya asubuhi alipokuwa anakwenda kuendesha misa katika Kanisa Katoliki la Betras lililopo eneo la Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, alikimbizwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na baadaye alifariki dunia.
Mwema alisema kutokana na kujirudiarudia kwa vitendo vya kuwashambulia na kuwadhuru viongozi wa dini na uchomaji wa nyumba za ibada, jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limeanza uchunguzi kuwabaini waliohusika na matukio hayo.
Aidha, alisema watu watatu wanashikiliwa kwa kuhusishwa na tukio la jana na kwamba majina yao hayawezi kutajwa hivi sasa kwa sababu za kiusalama.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment