Wednesday, June 26, 2013
AFRICA KUSINI YAJIANDAA NA KIFO CHA MANDELA
*Familia yake yakutana kwa dharura kijijini Qunu
*Yatembelea makaburi ya ukoo, wageni wazuiwa
SASA kuna kila dalili kuwa taifa la Afrika Kusini, limeanza kujiandaa kukabiliana na tukio zito la kifo cha Rais wa Kwanza wa Taifa hilo, Nelson Mandela (94), ambaye amelazwa kwa siku 18 hospitalini akisumbuliwa na maradhi ya mapafu. Kauli tofauti kuhusiana na mwenendo wa hali ya afya yake na matukio mbalimbali yasiyokuwa ya kawaida yanayoripotiwa kufanywa na familia yake, ndiyo ambayo yameamsha hisia hizo.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka nchini Afrika Kusini, zinaeleza kuwa watu muhimu katika familia ya Mandela, walikutana kwa dharura na kufanya mazungumzo ya faragha katika kijiji alichozaliwa cha Qunu.
Wakati wanafamilia hao wakikutana, msafara wa magari ya kundi jingine la wanafamilia, ulitembelea eneo la makaburi ya ukoo wa Mandela.
Eneo hilo la makaburi ya ukoo lipo mita chache kutoka yalipo makazi ya mdogo wake, Morris Mandela, mkabala na nyumba ya Mandela iliyoko kijijini Qunu.
Haikufahamika mara moja mazungumzo ya wanafamilia yalihusu jambo gani, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika Kusini, vililiripoti kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la Xhosa, wanafamilia hutembelea eneo la maziko iwapo kuna hisia za mmoja wa wanafamilia kufariki dunia na wakati mwingine kufanya tambiko la kimila.
Waliofika eneo la makaburi ni Winnie Madikizela-Mandela ambaye ni mke wa zamani wa Mandela, Waziri wa Utumishi wa Umma, Lindiwe Sisulu na Kiongozi wa chama cha upinzani cha United Democratic Movement, Bantu Holomisa.
Msafara wao ulifika eneo la makaburi jana asubuhi na kulikuwa na taarifa kuwa mtoto wa kike wa Mandela, Makaziwe Mandela, aliitwa eneo hilo.
Waandishi wa habari walizuiliwa kuvuka geti la eneo la makaburi hayo na waliofika nyumbani kwake Qubu, walipigwa marufuku kusogea karibu na nyumba hiyo.
Wanafamilia walioripotiwa kukutana kijijini Qunu ni Mandla Mandela, Thanduxolo Mandela, Ndaba Mandela na Ndileka Mandela na Chifu Bhovulengwe wa Baraza la AbaThembu.
Kikao hicho kinaeleza kuketi kuanzia saa nne asubuhi, lakini baadhi ya wanafamilia waliotakiwa kukihudhuria walichelewa kwa sababu ya kutopata taarifa mapema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment