.
MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ''Sugu" (Chadema), alikamatwa na
polisi mjini hapa jana na kuhojiwa kwa saa mbili na nusu, akidaiwa
kumtukana Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupitia mtandao wa jamii wa
‘facebook’. Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime,
alisema Sugu alikamatwa saa 8.00 mchana akitokea bungeni na kufikishwa
katika Kituo cha Polisi cha kati kwa mahojiano.
Misime alisema polisi waliamua kumkamata mbunge huyo baada ya
kugundulika kuandika maneno ya kumtukana Waziri Mkuu juu ya utendaji
wake.
Mbunge huyo anadaiwa kumtukana Waziri Mkuu kufuatia kauli
yake aliyoitoa hivi karibuni bungeni, katika kipindi cha maswali ya papo
kwa papo.
Katika kauli yake hiyo, Pinda alivitaka vyombo vya
dola ikiwemo Jeshi la Polisi kutowavumilia watu wanaotishia amani na
utulivu hapa nchini.
"Ni kweli tulimkamata Sugu majira ya saa
nane mchana na alihojiwa kuhusiana na tuhuma hizo, lakini alidhaminiwa
na Tundu Lissu akiwa na mwalimu mmoja wa Sekondari ya Viwandani majira
ya saa 10.30 jioni," alisema Misime.
"Hata hivyo mbunge huyo
analazimika kufika tena kesho (leo) saa tatu asubuhi, kwa ajili ya
kuendelea na mahojiano zaidi kuhusiana na kauli yake katika mtandao huo"
alisisitiza Misime.
"Kwa leo (jana), tumekamilisha taratibu zetu
ila tutaendelea kwa hatua zaidi kesho (leo), mara atakapofika kwani
anatakiwa kufika asubuhi kesho," alisema Misime.
Mkuu huyo wa
Jeshi la Polisi mkoani hapa, alisema Polisi itaendelea kumchukulia hatua
zaidi kadiri itakavyoona inafaa, ikiwemo kumpeleka katika vyombo vya
sheria.
Kamanda alisema Polisi haitasita kumkamata mtu yeyote
ambaye ataonyesha kupandikiza mbegu za chuki ambazo zinaweza kuvunja
amani na utulivu wa nchi na kuwataka watumiaji wa mitandao hiyo kuitumia
kwa minajiri iliyokusudiwa na si kutukana.
Hivi karibuni
kumezuka tabia ya baadhi ya wanasiasa kutumia mitandao ya kijamii
kuwachafua watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wa serikali kwa manufaa
yao.
Kauli ambazo zimekuwa zikiandikwa na kuwekwa katika mitandao
hiyo, zimekuwa zikijenga chuki kati ya wananchi na serikali yao ikiwemo
viongozi.
No comments:
Post a Comment