Binti huyo mwenye umri wa miaka 15 ambaye ni mkazi wa kitongoji cha
Mbugani katika kijiji cha Mkaramo, wilayani humo, alilazimika kukimbia
kwao na kwenda kulala kichakani baada ya kulazimishwa kuacha shule ili
aolewe wakati mwenyewe anataka kutimiza ndoto zake za kuendelee na
masomo.
Akizungumza jana akiwa katika eneo la ofisi za mkuu wa
wilaya ya mjini Handeni, Binti huyo alisema kwamba tukio hilo lilitokea
juzi majira ya mchana kijijini hapo, kufuatia babu yake kutaka kumchapa
viboko kumlazimisha aolewe.
Alieleza kwamba, aliamua kuchukua uamuzi huo mgumu baada ya kuona
akifikisha suala hilo kwa serikali ya wilaya hiyo ambayo amesikia ina
mradi wa kukomboa wasicha unaoitwa ‘Niache Nisome’ atasaidiwa ili aweze
kusoma.
“Mimi ninaishi kwa Babu yangu huko Mbugani Mkaramo, alitaka
kuniozesha mwanaume ambaye wala sijawahi kumuona, lakini nadhani naye ni
Mmang’ati. Alitaka niache shule ili niolewe, nikamkatalia kwavile
nataka nisome, alivyoona vile alitaka kunipiga,” alisema binti huyo na
kuongeza.
“Niliamua kukimbilia kujificha porini majira ya saa 5:00 asubuhi
hadi saa 10 usiku, nikapanda gari ya kwenda Mkata, nilipofika huko
nikapata gari nyingine iliyonifikisha kwa Mkuu wa Wilaya. Lengo langu ni
kuomba msaada serikali inisaidie nisome au ikibidi niweze kufika kwa
ndugu zangu Dodoma ili nisome,” alisema.
Agnes ambaye ni mmoja kati ya watoto wanne wa familia yao ndiye
pekee anayesoma na alieleza kwamba wazazi wake wote walifariki dunia
miaka mingi, ambapo mama yake alifia mkoani Dodoma.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo
Rweyemamu, alisema kwamba anaona faraja kubwa mafaniko yanayopatikana
katika mradi wa Niache Nisome ambao umeanzishwa kwa ajili ya kumkomboa
mtoto wa kike dhidi ya mimba na ndoa za utotoni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM wilayani
Handeni, Athumani Malunda, pamoja na Katibu wake Salehe Kikweo ambao
walishuhudia tukio hilo, walimpongeza binti huyo kwa ujasiri aliouonesha
katika msimamo wake wa kutaka kusoma.
No comments:
Post a Comment