Wamiliki wa vituo vya utangazaji nchini wameomba kuruhusiwa kwa muda
matumizi ya mfumo wa utangazaji wa analojia na digitali ili wananchi
wasiokuwa na uwezo waendelee kupata habari kupitia luninga.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, walisema
kuwa kuharakishwa kwa uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya analojia
nchini kunawakosesha wananchi wengi wa kipato cha chini haki ya kikatiba
ya kupata habari kupitia televisheni kwa kushindwa kumudu bei ya
ving’amuzi, huku vituo vya televisheni vikikabiliwa na hatari ya
kufungwa kutokana na kupungua kwa kasi ya matangazo ya biashara.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT),
Dk. Reginald Mengi, alisema kuwa mfumo wa sasa wa digitali
unaowalazimisha wananchi wote kupata matangazo ya televisheni kupitia
ving’amuzi unawakosesha wengi matangazo hayo na matokeo yake, wamiliki
wa vituo vya TV wanathirika kutokana na watangazaji kupunguza matangazo
yao na hivyo kuvikosesha vituo hivyo fedha za kuendeshea shughuli zao
kupitia matangazo ya kibiashara kama ilivyokuwa zamani.
Dk. Mengi ambaye alifuatana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Media Group
Ltd (Star TV), Samwel Nyalla na Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa
Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, alisema ana matumaini kuwa kilio chao
kitasikilizwa mapema ili kuwawezesha wananchi wa kawaida kupata habari
na vituo vya televisheni kupata matangazo ya biashara ya kutosha
yatakayowapatia fedha za kugharimia uendeshaji.
“Wananchi wengi ni walalahoi ambao hawana uwezo wa kulipia ving’amuzi.
Sisi kama wamiliki wa vituo vya TV tunapata hasara kwani hatuapati
matangazo ya kutosha tunapotazamwa na watu wachache,” alisema.
Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP inayomiliki vituo vya
tv vya ITV, EATV na Capital TV, aliongeza kuwa bado wanaendelea kufanya
taratibu za kuisihi serikali itekeleze yale wanayoomba na kwamba
wataendelea kufanya subira kwa miezi kati ya miwili hadi mitatu kuanzia
sasa na wakiona kuwa bado serikali iko kimya, watakachokifanya ni
kufunga vituo vyao vyote vya televisheni na kuendelea na biashara
nyingine.
“Tumekuwa tukijadiliana na wahusika kwa njia zisizo rasmi, lakini bado
tatizo lipo. Miezi miwili au mitatu ijayo hatutaona tv labda TBC (TV ya
Taifa). Kama huo ndiyo ulikuwa mpango wa kuondoa tv, basi wamefanikiwa.
Lakini naamini lengo lao lilikuwa kuboresha matangazo ya tv. Kwanini
ifanywe haraka hivyo?” alihoji Dk. Mengi.
Alisema kuwa wadau wa tv walishirikishwa na TCRA katika hatua za kuhama
kutoka analojia kwenda dijitali, lakini hawakuhusishwa katika kuamua
muda na utaratibu wa uzimaji wa mitambo ya analojia.
“Hatua ya kuhama ina madhara makubwa sana. Kinachosikitisha zaidi, nchi
tajiri hawakufanya haraka kuingia katika mfumo huu, USA (Marekani)
walitumia miaka 14, UK (Uingereza) miaka 11, Hispania miaka 10 na Japan
miaka minane. Sisi tumetumia muda mfupi sana,” alisema.
“Hakuna msaada wowote unaotoka serikalini kuwawezesha Watanzania wenye
hali duni kiuchumi kumudu gharama za ving’amuzi. Huku ni kuwanyima haki
ya kupata habari wananchi ambayo ni ya kikatiba kwani Ibara ya 18 ya
katiba yetu inatamka wazi kuwa wananchi wana haki ya kupata habari.
“Mambo yanayofanywa nchini lazima yaangalie hali halisi ya maisha ya
Watanzania. Watanzania wametumbukia kwenye giza; giza la kutopata
habari. Ombi letu kwa serikali ni kurudisha mfumo wa analojia uende
sambamba na mfumo wa digitali wakati watu wanajipanga vizuri zaidi.”
MTENDAJI MKUU SAHARA
Kwa upande wake Nyalla alisema kuwa wameshangaa kuona Tanzania inazima
mitambo ya analojia huku hali ya uchumi wa wananchi wake ikiwa duni na
kwamba baadhi ya vituo vya tv hasa vya mikoani vimefungwa kwa vile
haviwezi kumudu uendeshaji wa mfumo mpya wa utangazaji wa digitali.
Nyalla alisema kuwa kituo chake cha Stars TV, kimekumbwa na tatizo la
kupungua kwa matangazo hali ambayo imeathiri shughuli za uendeshaji.
“Tumekimbilia kwenye digitali kwa faidi ipi hasa?” alihoji na kuongeza:
“Tunajiuliza kwa nini hasa kuna kitu hiki. Hakuna ruzuku ambao sisi
wamiliki wa vyombo wa habari binafsi tunaoupata kutoka serikalini
kusaidia kuinua mipango ya vituo vyetu.”
Mkurugenzi huyo aliendelea kueleza kuwa idadi ya ving’amuzi ambavyo hadi
sasa vimo nchini ni kati ya 500,000 na 600,000, idadi ambayo
inamaanisha kwamba Watanzania wengi hawatazami tv kwani idadi ya
Watanzania ni zaidi ya milioni 44 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka jana.
MKURUGENZI CLOUDS
Naye Mutahaba alisema vituo vya tv nchini bado havijaandaliwa vyema
kukabiliana na ushindani wa habari na tv za mataifa ya nje katika mfumo
mpya wa utangazaji wa digitali.
“Kutokana na hali halisi ya uendeshaji wa vyombo vyetu, bado hatuna
uwezo wa kushindana na mataifa ya nje. Kulipia kodi ya matangazo ndani
ya nchi yetu inakuwa vigumu,” alisema Ruge.
Kwa mujibu wa Ruge, gharama ya kupeleka matangazo ya tv kwa kila mkoa
nchini ni Dola za Marekani 3,800 (Sh. milioni sita) kwa mwezi.
TCRA WANENA
Alipotafutwa na NIPASHE jana, Meneja wa Mawasiliano wa TCRA, Innocent
Mungy, alisema kuwa maamuzi ya Tanzania kuingia kwenye mfumo wa
utangazaji wa digitali ni makubaliano ya kimataifa huku akisisitiza kuwa
kila nchi lazima iingie katika mfumo.
“Suala la digitali ni la kimataifa, kila nchi lazima itumie mfumo huo.
Ombi la wamiliki wa vyombo vya habari kuhusu analojia siwezi
kulizungumzia kwa sasa kwa sababu ni la kiserikali, halipo kwenye
mamlaka hii. Nafikiri waulize Maelezo (Idara ya Habari), wao ndiwo
watatoa tamko la serikali,” alisema Mungy.
Alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia suala hilo jijini Dar es Salaam
jana, Mkurugenzi wa Maelezo, Assah Mwambene, alisema kuwa maombi ya
wamiliki wa vyombo vya habari (TV) hadi jana saa 12:25 jioni yalikuwa
hayajawasilishwa rasmi kwenye ofisi yake.
“Hatujapokea barua rasmi ya maombi yao. Wakituandikia tutawajibu,” alisema Mwambene.
Serikali ililazimisha kuanza urushaji wa matangazo kupitia mfumo wa
ving’amuzi kuanzia Januari Mosi, 2013 na kuzima kwa awamu matangazo yote
ya televisheni kupitia njia iliyokuwa ikitumika awali ya analojia
isiyohitaji ving’amuzi bali antena za kawaida.