*Familia yake yakutana kwa dharura kijijini Qunu
*Yatembelea makaburi ya ukoo, wageni wazuiwaSASA
kuna kila dalili kuwa taifa la Afrika Kusini, limeanza kujiandaa
kukabiliana na tukio zito la kifo cha Rais wa Kwanza wa Taifa hilo,
Nelson Mandela (94), ambaye amelazwa kwa siku 18 hospitalini
akisumbuliwa na maradhi ya mapafu. Kauli tofauti kuhusiana na mwenendo
wa hali ya afya yake na matukio mbalimbali yasiyokuwa ya kawaida
yanayoripotiwa kufanywa na familia yake, ndiyo ambayo yameamsha hisia
hizo.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka nchini Afrika Kusini, zinaeleza
kuwa watu muhimu katika familia ya Mandela, walikutana kwa dharura na
kufanya mazungumzo ya faragha katika kijiji alichozaliwa cha Qunu.
Wakati
wanafamilia hao wakikutana, msafara wa magari ya kundi jingine la
wanafamilia, ulitembelea eneo la makaburi ya ukoo wa Mandela.
Eneo hilo la makaburi ya ukoo lipo mita chache kutoka yalipo makazi
ya mdogo wake, Morris Mandela, mkabala na nyumba ya Mandela iliyoko
kijijini Qunu.
Haikufahamika mara moja mazungumzo ya wanafamilia
yalihusu jambo gani, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika
Kusini, vililiripoti kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la
Xhosa, wanafamilia hutembelea eneo la maziko iwapo kuna hisia za mmoja
wa wanafamilia kufariki dunia na wakati mwingine kufanya tambiko la
kimila.
Waliofika eneo la makaburi ni Winnie Madikizela-Mandela
ambaye ni mke wa zamani wa Mandela, Waziri wa Utumishi wa Umma, Lindiwe
Sisulu na Kiongozi wa chama cha upinzani cha United Democratic Movement,
Bantu Holomisa.
Msafara wao ulifika eneo la makaburi jana
asubuhi na kulikuwa na taarifa kuwa mtoto wa kike wa Mandela, Makaziwe
Mandela, aliitwa eneo hilo.
Waandishi wa habari walizuiliwa
kuvuka geti la eneo la makaburi hayo na waliofika nyumbani kwake Qubu,
walipigwa marufuku kusogea karibu na nyumba hiyo.
Wanafamilia
walioripotiwa kukutana kijijini Qunu ni Mandla Mandela, Thanduxolo
Mandela, Ndaba Mandela na Ndileka Mandela na Chifu Bhovulengwe wa Baraza
la AbaThembu.
Kikao hicho kinaeleza kuketi kuanzia saa nne
asubuhi, lakini baadhi ya wanafamilia waliotakiwa kukihudhuria
walichelewa kwa sababu ya kutopata taarifa mapema.