Thursday, December 27, 2012

WATU WAWILI WAUAWA MBEYA CHRISTMAS

Watu wawili wameuawa katika matukio tofauti mkoani Mbeya wakati wa sikuu ya Krismas likiwamo tukio la kijana mmoja kumuua kaka yake kwa kumchoma kisu.

Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alisema kuwa katika tukio la kwanza lililotokea majira ya saa 2:00 asubuhi katika maeneo ya Sae Jijini Mbeya, mtu mmoja ambaye bado hajafahamika, aliuawa na wanachi wenye hasira baada ya kumtuhumu kuwa ni mwizi.

Alisema kuwa mtu aliyeuawa ni kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 20 na 25 ambaye alishambuliwa kwa marungu na mapanga hadi mauti yalipomfika.

Kamanda Diwani alisema kuwa baada ya mauaji hayo, watu waliokuwa wakimshambulia walitoweka na kuwa hadi sasa Jeshi la Polisi halijagundua marehemu alitaka kuiba nini wala mahali alipotuhumiwa kuiba.

Katika tukio la pili lililotokea wilayani Rungwe, Kamanda Diwani alisema kuwa kijana Itamu Mwakagenda (23) aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani na ndugu yake aitwaye Nebo Daudi maarufu kwa jina la Isalikila wakati wakigombea panga.

Kamanda Diwani alisema kuwa majira ya saa 12:00 asubuhi wakati watu wakijiandaa kwenda kanisani, kuliibuka ugomvi miongoni mwa wanandugu hao kila mmoja akihitaji panga ili alitumie kwa shughuli zake.

Alisema ugomvi huo ulisababisha Nebo mwenye umri wa miaka 21 kuchukua kisu alichokitumia kumchoma kifuani kaka yake na kumsababishia kifo papo hapo.

Alisema baada ya mauaji hayo Nebo alitoroka na kuwa hadi sasa Jeshi la Polisi linaendelea na msako dhidi yake ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Aidha, Kamanda Diwani alisema kuwa mbali na matukio hayo ya mauaji, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu 16 waliokamatwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za kukutwa na bangi na unywaji wa pombe haramu ya gongo.

No comments: