Sunday, January 27, 2013

MTWARA KUMEWAKA MOTO WATU WAUAWA

Watu wauawa, majeruhi kibao, 30 mbaroni
Ofisi za serikali, shule, mahakama, magari 11, vyateketezwa





Watu wanne wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa kufuatia vurugu kubwa zinazoendelea katika mji wa Masasi, mkoa wa Mtwara zilizoambatana na uchomaji moto wa majengo ya serikali, magari na nyumba za viongozi.

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo, hata hivyo majina ya waliokufa hayakuweza kupatikana mara moja.

Alisema kati ya watu waliojeruhiwa yumo askari mmoja ambaye amelazwa katika hospitali ya Ndanda.

Waliojeruhiwa wametajwa kuwa ni Hosea Kibona (polisi), Mohamed Abilai, Amami Ali, Athuma Maelezo, Zaruki Mussa, Mohamed Mshamu, Nassoro Mohamed, Yona Mareme, Feti William, William Matiponi, Jarome Frank na Maisha Hussein, ambaye ana risasai shingoni. Majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya, Ndanda.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Crisprin Sapuli, amethibitisha kupokea majerehi hao ambao kati yao wanne hali zao ni mbaya akiwemo polisi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika eneo la tukio, vifo hivyo vimetokana na risasi zilizokuwa zikipigwa hewani wakati polisi wakijaribu kutuliza vurugu hizo baada ya mabomu ya machozi kushindwa kuwatanya wananchi hao.

Vurugu hizo zinadaiwa kusababishwa na maandamano ya kundi la vijana lililokuwa likielekea Ofisi ya Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ilala baada ya askari aliyekuwa akiendesha pikipiki kumgonga mtembea kwa miguu na kumvunja mguu.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo waliliambia Gazeti hili kuwa baada ya mtu huyo anayedaiwa kuwa ni dereva wa bodaboda kugongwa jana asububi kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam –Tunduru, askari huyo aliondoka bila kutoa msaada.

Wananchi walioshuhudia tukio hilo walidai kuwa kundi hilo la vijana ambao linasadikiwa pia ni la madereva wa bodaboda lilimsaidia majeruhi huyo kwa kumpeleka kituo cha polisi cha wilaya ili kupata fomu ya PF3 kwa ajili ya matibabu katika hospitali ya Mkomahindo.

Hata hivyo, walidai walipofika kituoni hapo hawakupata ushirikiano kutoka kwa polisi waliokuwa kituoni.

Kufuatia hali hiyo ndipo wananchi walipojikusanya na kufanya maandamano kuelekea Kituo cha Polisi cha Wilaya kwa ajili ya kuonana na Kamanda wa Polisi wa Wilaya.

Hata hivyo, wananchi hao hawakuweza kumuona kamanda huyo kitendo kilichowafanya

Wananchi hao kusambaa maeneo ya mji wa Masasi na kuanza kufanya fujo za kuchoma matairi kwenye barabara zote za Masasi – Tunduru na Nachingwea – Masasi.

Aidha, waliekea Soko Kuu la Masasi na kuchoma moto kituo kidogo cha polisi Mkomahindo na baadae waliekea nyumbani kwa Mbunge wa Masasi Mjini (CCM), Mariamu Kassembe, kuvunja milango, kuingia ndani na kuchukua vitu mbalimbali na kisha kuchoma moto gari lake lenye namba za usajili T497 APE, trekta moja na kontena lililokuwa na vifaa mbalimbali vya ujenzi.

Kassembe alithibitisha kutokea kwa hali hiyo wakati akiongea na Gazeti hili jana.

Kundi hilo pia lilielekea katika nyumba na shule inayomilikiwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Anna Abdallah na kuzichoma moto.

Mbali na nyumba hizo, kundi hilo pia lilichoma moto ofisi ya CCM, ofisi ya Maliasili, Mahakama ya Mwanzo, kituo cha polisi na Ofisi ya Elimu ya wilaya.

Aidha, katika vurugu hizo magari 11 mali ya halmashauri ya wilaya hiyo yamechomwa moto.

Kundi hilo pia lilikwenda kwenye nyumba za askari polisi wanaoishi uraiani na kuingia nyumba moja baada ya nyingine kwa nia ya kuzichoma.

Katika vurugu hizo nyumba mbili ikiwemo ya askari wa cheo cha Meja na askari wa kawaida zinadaiwa kuchomwa huku nyumba zingine zikiharibiwa mali zilizomo ndani.

Nyumba zingine ziliokolewa baada ya askari polisi kuingilia kati na kudhibiti watu hao.

Habari zilizopatikana kutoka katika eneo hilo zinasema kuwa askari polisi wa mkoa wa Lindi, waliingia mjini hapo kuongeza nguvu ya kudhibiti fujo hizo.

Kamishna pia amethibitisha kukamatwa kwa vijana zaidi 30 wanaotuhumiwa kuhusika katika fujo hizo na kushikiliwa katika kituo cha polisi Masasi.

Habari kutoka Masasi zinasema kukamatwa kwa vijana hao kulifanikiwa baada ya kuliteka gari moja kwa nia ya kuwapeleka wenzao waliojeruhiwa katika hospitali ya Ndanda.

Wakiwa njiani walikutana na Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao walilizuia gari hilo na kuwakamata.

Baadhi ya waliokamatwa ni Beatrice Steven (28), Hamis Saidi (24) na Ismail Msepe (26).

Habari zaidi zinaeleza kuwa katika vurugu hizo askari mmoja aliyekuwa kwenye kikosi kazi porini alivamiwa na kunyang’anywa bastola yake na kujeruhiwa vibaya.

Kamanda alisema magari mengine yaliyonusurika kuchomwa moto ni namba DPF 3064 na gari la Mkurugenzi wa Halmashauri namba SM 4409.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Farisa Mgomi, alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo na waandishi wa habari, alikataa kuzungumza.

Habari zinadai kuwa kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kilifanyika na kuwashirikisha polisi na maofisa usalama waliotoka Dar es Salaam.

Chagonja, amesema wito wao kwa wananchi ni kwamba waache kucheza na serikali kwa sababu ina nguvu, kama ni masuala ya gesi kuna mkutano uliitishwa ambapo wananchi walitoa malalamiko yao kwa wawakilishi wao ambao ni wabunge na kuyachukua ili kuyapeleka bungeni.

Alisema jeshi la polisi linashangaa kuona kabla ya wawakilishi hawajawasilisha mapendekezo yao bungeni, wameanza kuleta vurugu.

Kuhusu madai kuwa kunabaadhi ya askari polisi waliozuiliwa na wananchi wakati wakienda kuongeza nguvu Masasi, alikanusha na kueleza kwamba hakuna anayeweza kuwazuia na wanaweza kupasua popote wanapotaka kwenda.

No comments: