Monday, February 25, 2013

DALADALA YAUA WAWILI DAR NA KUJERUHI 46

http://www.cityguidetz.com/wp-content/uploads/2012/08/Dar-es-salaam.jpgAbiria wawili wamefariki dunia na wengine 46 kujeruhiwa katika ajali mbili zilizohusisha magari manne, zikiwamo daladala tatu walizokuwa wamepanda na Fuso, kugongana katika maeneo tofauti, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
 Kati ya waliofariki, mmoja ametambuliwa kwa jina la Sabrina Is-haka (11), ambaye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke.
Mwingine mwanaume, ambaye jina lake halijafahamika, anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30-31, alifariki dunia papo hapo katika eneo la ajali.
Mkuu wa askari polisi wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani Mkoa wa Temeke, Prackson Rugazia, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
 Pia Mwangalizi Mkuu wa jana wa Hospitali hiyo, Amosi Kaberege, alithibitisha hospitali yake kupokea majeruhi hao pamoja na miili ya watu waliofariki kuhifadhiwa hospitalini hapo. 
Kwa mujibu wa Kaberege, marehemu Sabrina, ambaye alikuwa na pacha mwenzake katika gari lililopata ajali, alifariki dunia kutokana na kutokwa na damu nyingi baada ya kukatika mguu.
 http://www.tanzaniatouristboard.com/gallery/uploads/posts/2008-03/thumbs/1204555029_dar-es-salaam-05.jpg
Aidha, kati ya waliojeruhiwa, 42, akiwamo pacha wa marehemu Sabrina, walitibiwa katika hospitali hiyo na kuruhusiwa.
 Hata hivyo, majeruhi wawili kati yao, walihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa Rugazia, ajali ya kwanza ilitokea katika Barabara ya Kilwa, eneo la Msikitini, Mtoni Mtongani, saa 12.30 asubuhi jana, ikihusisha daladala mbili aina ya Toyota DCM linalofanya safari zake Mwenge-Mbagala na Eicher la Mbagala-Kivukoni, yaliyogongana.http://www.tourtanzania.com/wp-content/uploads/2009/02/daressalaam1.jpg
Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya daladala aina ya Eicher lililokuwa likitokea Kivukoni kuacha njia na kwenda upande wa pili wa barabara na kuligonga daladala aina ya Toyota DCM lililokuwa likitokea Mbagala kwenda Mwenge.  
 Rugazia alisema dereva wa Toyota DCM, ambaye ni mmoja wa majeruhi alijisalimisha, lakini yule wa Eicher alikimbia baada ya ajali hiyo na kwamba, polisi wanaendelea kumsaka.
 Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na usukani wa Eicher kugoma kufanya kazi, hali iliyomfanya dereva wake kushindwa kulimudu gari hilo.
Aidha, kwa mujibu wa Kaberege, jana pia walipokea hospitalini hapo watu 11 waliojeruhiwa katika ajali iliyohusisha daladala aina Toyota Hiace iliyogongana na Fuso.
 Alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kwa Sokota, wilayani humo, majira ya saa 4 asubuhi. Hata hivyo, alisema watu hao walitibiwa na kuruhusiwa.

No comments: